“Nilizaliwa katika nyumba ile,” Marion Eden amesema, akionyesha nyumba ya ghorofa mbili ya matofali ya kuchoma iliyoko karibu. Eden, mwenye umri wa miaka 79, amekuwa akilima karibu na eneo la Elizabeth, Ill, maisha yake yote.
Baada ya kuvaa viatu vya shambani, Marion Eden mwenye umri wa miaka 79 alitembea mkabala na zizi la ng’ombe kuangalia ng’ombe wachache aina ya Black Angus waliojikusanya pamoja karibu na eneo la malisho.
Amekuwa akifanya shughuli za kilimo katika ardhi hii karibu na eneo la Elizabeth, Illinois, tangu akiwa miaka mitano.
“Mimi nilizaliwa katika nyumba ile,” amesema, akionyesha nyumba ya ghorofa mbili ya matofali iliyokuwa karibu.
“Enzi hizo, mtu ulikuwa unaanza kufanya kazi ukiwa mdogo, na nimeendelea kufanya kazi hii kwa takriban miaka 75 sasa, na wengi wanafanya kazi ya ufugaji ng’ombe,” amesema.
Yeye ana ng’ombe 25 hivi sasa na pia anakodisha baadhi ya ardhi yake kwa mkulima mwingine ili aweze kupanda maharage na mahindi. Zao pekee ambalo Eden anavuna ni majani, ambayo anatumia kuwalisha ng’ombe.
Mtoto pekee shambani
Kaka zake na dada zake wote wameacha kilimo, na sasa wanaishi sehemu mbalimbali nchini, wakiwa na watoto na wajukuu zao ambao wako mbali na eneo hilo la shamba lake.
“Ni lazima uwe na dhamiri ya kweli ya kufanya kilimo,” amesema. “Ni lazima uwe unapenda kilimo kwa muda mrefu ili uweze kufanikiwa kupiga hatua kubwa.”
Mzee huyu ana mtoto wa kike ambaye anaishi mjini na huwa anamtembelea na anafurahia hali ya mazingira ya kuvutia ya eneo hilo na pia nyota ambazo zimetanda angani wakati wa usiku.
Lakini Eden anaelewa kwa nini vijana wachache wanapendelea kujishughulisha na kilimo. Sio tu kwamba vijana wanavutiwa sana na maisha ya miji mikubwa, lakini kujishughulisha na kilimo ni gharama kubwa na kuna changamoto nyingi.
Kupata eneo la shamba ni vigumu kama kijana hajarithi ardhi au hana pesa ya kununua. Takriban asilimia 62 ya wakulima wa Marekani wana umri wa miaka 55 au zaidi.
Eden anasema kutokana na tabia ya biashara hiyo kuwa haina uhakika ambapo wakulima wanaweza kupoteza mazao kutokana na mafuriko au ukame, na kuadhibiwa na hali ya masoko iwapo watazalisha mazao zaidi ya mahitaji ya soko ambapo huangusha bei ya mazao.
Eden ana masikitiko makubwa juu ya wakulima vijana ambao wanataka kufanikiwa wakati mbolea, vifaa vya kilimo na ununuzi au ukodishaji mashine mbalimbali za kuvunia zinafanya iwe vigumu kufikia mafanikio.
“Iwapo mtu amepata mavuno mazuri,” Eden amesema, “itagharimu zaidi kuvuna kwa pamoja au kukausha nafaka, na kama akipata bei ya chini, ina maana kuwa pato lake litashuka sana kwa sababu ya gharama kubwa alizotumia.
Kuna programu ya serikali ya Marekani ambayo inawapatia wakulima bima kuwasaidia iwapo watafikwa na majanga yanayotokana na mazao kuathirika, ikiwa ni sehemu ya dola bilioni 20 au zaidi serikali kuu hutoa kwa wakulima kupitia ruzuku.
Lakini Eden anasema marupurupu ya kilimo yako juu lakini soko bado haliaminiki.
Kura ya mabadiliko
Wakulima, amesema, ni waconservative ambao siku zote wanawapigia kura warepublican, lakini kuna wademokrat katika miji mikubwa kwenye kaunti ya Jo Daviess, na walimsaidia Rais Barack Obama kushinda kaunti hiyo mwaka 2012.
Lakini uchaguzi wa Novemba mwaka jana, kura nyingi zilikwenda kwa Donald Trump, ikimaanisha kuwa baadhi ya wafuasi wa Obama walibadilisha vyama vyao.
“Nafikiri watu walikuwa wanapiga kura kwa ajili ya mabadiliko,” Eden amesema. “Hajalishi vipi wamepiga kura katika siku zilizopita, ilikuwa kwa sababu ya mabadiliko.”
Eden anafuatilia habari, lakini anasema mambo mengi yanayozungumziwa katika ngazi ya kitaifa inaonekana ni mageni yakiangaliwa kwa mtizamo wa wale walioko shamba upande wa kaskazini magharibi huko Illinois.
Ugaidi, kwa mfano, unamtia wasiwasi kama Mmarekani na kwa sababu ana watu ambao anawapenda katika maeneo mengine ya nchi. Lakini amesema, “Kuishi hapa, sina kitu ambacho kinanitia wasiwasi.’
Marion Eden, ambaye ana jishughulisha na kilimo nje ya eneo la Elizabeth, III, anaelewa kwa nini vijana wachache wanajiingiza katika kilimo hivi leo.
“Ni lazima uwe unataka kushughulika na kilimo,” amesema. “Ni lazima uwe unapenda kilimo kwa kipindi kirefu ili uweze kupata mafanikio makubwa.”
Na hivyo hivyo katika uhamiaji, kitu ambacho hakina athari yoyote katika eneo hili.
Aina ya kilimo kinachoendelea hapa hakitegemei upatikanaji wa vibarua kama ilivyo maeneo mengine ambako wahamiaji wanatumika katika kilimo.
Wahamiaji wachache wanaoishi katika kaunti ya Jo Daviess wengi wao wanafanya kazi katika mahoteli na migahawa katika eneo la Galena, mji wa kitalii ambako viongozi wake wanajadiliana jinsi gani wanataka mji wao uwe unawavutia wageni, wakati uongozi wa Trump ukilenga “miji hiyo yenye kutoa hifadhi” kwa wale ambao hawatoisaidia serikali kuu kuwakamata watu waliokiuka sheria za uhamiaji.
Lakini ingawaje Galena ni mwendo wa nusu saa kwa gari kutoka mjini, kinachotokea ni kuwa hakuna tofauti kubwa kwa wale watu wanaoishi nje ya mji.
Eden, ambaye huongeza kipato chake akifanya kazi kwenye kampuni ya bima ya kilimo amesema hajihusishi na siasa.
Kuhusu kilimo, akiwa anaelekea kuwa miaka 80, amesema ana mpango wakuendelea na kilimo kwa kadri afya yake itakavyo mruhusu.