Ron Gruenhagen, mkulima kutoka Muscatine, Iowa, anasema wakulima wa Marekani wanategemea zaidi masoko ya nje. “Ingekuwa hatuna haya masoko ya kigeni tungeelemewa na wingi wa nafaka na maharage ya soya na pengine tusingejua cha kufanya na mazao haya,” amesema.
Ron Gruenhagen mwenye umri wa miaka 73 ni katika kizazi cha wahamiaji waliotokea Ujerumani ambao walikuja jimbo la Iowa katikati ya karne ya 19.
Muscatine na kaunti zinazo zizunguka Iowa na Illinois zilikuwa ndio sehemu kubwa walizozielewa duniani siku hizo na mazao mengi waliyokuwa wanazalisha yalikuwa yananunuliwa na watu wa maeneo ya karibu.
Hivi leo, baadhi ya operesheni zinadhibitiwa na sheria zilizopitishwa Washington, na wanunuzi wengi wa mazao hayo wako mbali huko nchini China.
“Tunategemea zaidi masoko ya kigeni,” amesema. “kama tungekuwa hatuna hayo masoko tungekuwa tumeelemewa na nafaka na maharage ya soya na pengine tusingejua nini cha kufanya.”
Wasiwasi wa vita ya kibiashara
Rais Donald Trump ameahidi kufanya mashauriano mapya juu ya mikataba ya kibiashara iliyokuwepo ambayo ameyaelezea ni makubaliano mabaya kwa upande wa Marekani na ameiondoa kutoka katika ushirikiano wa mazungumzo ya Trans Pacific Partnership (TPP) ambayo yalikuwa yamelenga kukuza biashara kati ya Marekani na nchi nyingine 10.
Wakulima wengi katika eneo hilo na viongozi wa biashara wanahofia kuhusu vita vya kibiashara vitavuruga biashara na nchi kama vile China, Mexico na mataifa mengine ambayo yamekuwa ni washirika wa karibu wa kibiashara.
Lakini Gruenhagen anaona msimamo mkali wa Trump ni sehemu ya mkakati wa kufanya majadiliano.
“Inanipa wasiwasi, lakini yote hayo ni sehemu ya mashauriano,” amesema. “Kila kitu tunachofanya kimezungumziwa, iwapo unanunua mkate dukani au unanunua trekta, vyote vinapatikana kupitia mazungumzo.
Mahusiano ya muda mrefu na China
Kaunti ya Muscatine, Iowa, ina mahusiano maalum na China kwa sababu Rais wa China Xi Jinping aliishi katika familia ya kimarekani mwaka 1985 wakati akiwa afisa wa jimbo aliyekuwa na hamu ya kujifunza zaidi kuhusu kilimo cha Marekani.
Aliporudi kwa ajili ya ziara yake kama makamu wa rais mwaka 2012, wengi kati ya watu aliokuwa amekutana nao siku hizo walikuja kumsalimia.
Kamati maalum ya kumkaribisha, ilikuwa na viongozi wa biashara wa eneo hilo ambao baadae waliendeleza ushirikiano madhubuti ulioanzishwa kati ya Muscatine na China, ambao ulikuwa unasukuma mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya kaunti na kampuni za Kichina.
Hivi karibuni mji wa Muscatine uliandaa tafrija kwa ajili ya Gavana wa Iowa, Terry Branstad, ambaye Rais Trump amemchagua kuwa Balozi wa Marekani nchini China. Shughuli hiyo ilihusisha bendi ya kichina iliyokuwa imeandaliwa na ubalozi mdogo wa China huko Chicago.
Gruenhagen anafikiria ni kitu chenye maslahi kuwa na kiongozi mchina ambaye anaijua Iowa na vijiji vya Marekani kutokana na uzoefu wake wa kuwa ameishi katika maeneo hayo.
“Bila shaka anaelewa shughuli za kilimo za eneo hili na hiyo ni nusu ya ushindi wa vita katika mazungumzo ya kibiashara — kuwafahamu watu unaozungumza nao,” amesema.
Hana shaka kuwa kunaweza kukatokea mvurugano wa kibiashara, pamoja na Trump kuchukuwa msimamo mkali.
Ilivyokuwa kwamba tumekuwa tunategemeana, wao wanategemea chakula chetu na sisi tunahitaji bidhaa zao wanazotuletea, tunategemeana na hilo ni muhimu sana, pengine kwa ajili ya kuendeleza amani ulimwenguni,” amesema.
Gruenhagen anaamini Trump atabadilisha kile anachokiona kuwa ni kuporomoka kwa nafasi ya Marekani ulimwenguni.
“Tumepoteza nafasi yetu ambayo tuliokuwa tunayo kama taifa bora lenye nguvu,” amesema.
Pengine tunaweza bado tukaitwa taifa lenye nguvu, lakini kwa hivi karibuni hatujaendelea kuitwa taifa kubwa. Nafikiri tutarudi katika nafasi yetu ya juu na kupata heshima hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzoni.”
Kupunguza kanuni
Ana matumaini kuwa uongozi wa Trump unaosaidiwa na wabunge wa Republican utaweza kuondoa mzigo wa kanuni za biashara, viwanda and kilimo, na amesisitiza kuwa shirika la Kulinda Mazingira, ndio mhalifu mkubwa zaidi. Uongozi huu unaonekana unataka kuliangamiza shirika hilo.
“Kanuni hizi zinatunyonga,” amesema. “Inatuchukulia muda wetu mwingi katika kuweza kuhakikisha tunafuata hizi sheria.”
Ingawaje anapendelea na njia za kilimo ambazo zinalinda mazingira na kuhifadhi udongo, Gruenhagen haamini kuna umuhimu wa serikali kuu kuwaambia wakulima huko Iowa nini cha kufanya.
“Nafikiri ni bora kwa kila mkulima kuamua kile kilicho bora katika shamba lake, jinsi gani azuie mmomonyoko wa udongo na jinsi ya kufanya ardhi iwe bora kuliko kuwa na afisa wa serikali kutoka Washington DC kutuainishia nini ndio kitu bora kwetu,” amesema.
Na bado wanamazingira hawana matumaini makubwa, wakidai biashara kubwa za kilimo za kimataifa ambazo wafanya maamuzi wanaishi sehemu nyingine ambapo wao wanajali zaidi faida na sio ardhi.
Mtoto wa kiume wa Gruenhagen na mjukuu wake wa kiume wanamsaidia katika shughuli za shamba lake, na ana furaha kuweza kuendeleza jina la familia wakati watakapo rithi ardhi, majengo na vifaa vvenye thamani ya dola za Marekani milioni moja.
“Hii ni kazi kubwa,” amesema, “lakini ni furaha yangu kwa sababu tunakuwa na uwezo wa kuwalisha watu wengi na ndiyo, pia tunalisha ulimwengu.”